PROACTIVE LAW ENFORCEMENT FOR SAFE COMMUNITY Usalama Barabarani
Usalama Barabarani

Ajali za barabarani zimezidi kua miongoni mwa vyanzo vikubwa vinavyo chukua uhai wa watu wengi na kusababisha majeraha na ulemavu kwa maelfu ya watu. Umoja wa mataifa na shirika la afya duniani wanakadiria kua watu zaidi ya milioni 1.3 hupoteza maisha kila mwaka, idaidi hii ikiwa ni mara mbili ya vifo vinavyosababishwa na Malaria na UKIMWI. Vifo vingi na majeraha hutokea zaidi katika nchi za uchumi wa kati na zinazoendelea kama Tanzania.

 

Shabaha ya malengo ya maendeleo endelevu (Sustainable Development Goals) pamoja na muongo wa pili wa hatua kwa ajili ya usalama barabarani (Second Decade of Action for Road Safety 2021-2030) kidunia ni kupunguza kwa asilimia 50% vifo na ulemavu unausababishwa na ajali za barabarani ifikapo mwaka 2030.

 

Kwa upande wa Tanzania, dira ya maendeleo 2025 inalenga kuongeza umri wa kuishi wa watanzania na kufikia Tanzania ya uchumi wa kati wenye ushindani huku vijana wakiwa ni tegemeo kubwa zaidi. Lakini ajali za barabarani zimekua zikiathiri na kugharimu maisha watu, wengi zaidi wakiwa ni vijana na watoto. Mamlaka husika pamoja na wadau wamekua wakifanya jitihada kukabiliana na ajali za barabarani. Mbali na jitihada hizo ajali za barabarani zimeendelea kujitokeza na kuwa tatizo linalogharimu maisha ya watanzania wengi. Takwimu zinaonyesha kwa mwaka 2020 idadi ya matukio na ajali za barabarani ilikua ni zaidi ya milioni 2.1, huku vifo pekee vikiwa ni 1,384. Hii ikimaanisha kwa mwaka 2020 watu zaidi 115 walikua wanafariki kila mwezi kutokana na ajali za barabarani.

 

Ili kukabiliana na tatizo la ajali za barabarani PESACO imejizatiti kuunga mkono jitihada za serikali na vyombo vyake katika kuhakikisha tunafikia Tanzania isio na ajali. Tukitumia nyenzo ya elimu PESACO inayafikia makundi yote sita ya watumia barabara, kuwapa elimu stahiki itakayowasaidia kudumisha uwiano wa matumizi salama ya barabara ili kuepukana na ajali.

 

Usalama barabarani umesimama kwenye nguzo kuu tatu ambazo ni:-

 

 1. Ubora na uzima wa barabara (Engineering)  
 2. Usimamizi wa sheria za barabara (Enforcement)  
 3. Elimu ya usalama barabarani (Education)

 

PESACO imejikita kwenye nguzo moja ya elimu ya usalama barabarani, na katika utoaji wa elimu tunalenga mambo makuu matatu(3) ambayo ni:-

 

 1. Kukuza maarifa na uelewa wa sheria za barararani na mazingira yake
 2. Kuongeza ujuzi kupitia mafunzo na uzoefu
 3. Kuimarisha na kusisitiza mitazamo chanya wakati wa kutafsiri mazingira hatarishi barabarani, kujilinda binafsi na kuwalinda watumiaji wengine wa barabara

 

Katika kufanikisha malengo hayo ya utoaji wa elimu ya usalama barabarani, PESACO inatoa elimu hii kwa watumiaji wote sita wa barabara, amabo ni, wenye vyombo vya moto (magari, tela, pikipiki na bajaji), watembea kwa miguu, wapanda baiskeli, wasukuma mikokoteni, waswagaji wanyama, waendesha maguta. Majukumu yetu tunayatimiza kwa kuonana na wahusika ana kwa ana na kwa kutumia vitabu, vipeperushi, makala na matangazo mbalimbali. Njia tunazotumia kutoa elimu ni kama:-

 

 1. Kuita na kuandaa semina za elimu kwa madereva na wafanyakazi wa taasisi za serikali na binafsi. Elimu hii inatolewa moja kwa moja kwa kufika maeneo husika.
 2. Kufika kwenye shule za msingi na sekondari kwa lengo la kuwapa wanafunzi na walimu elimu, ujuzi na maarifa ya usalama barabarani.
 3. Kufika kwenye vituo vya bodaboda na bajaji na kutoa elimu ya usalama barabarani
 4. Kufika kwenye vituo vya mabasi na daladala kwa lengo la kutoa elimu kwa abiria pamoja na madereva
 5. Kufika ofisi za serikari na binafsi kwa lengo la kutoa vitabu, makala na vipeperushi vya usalama barabarani
 6. Kuandaa mabonanza ya michezo kwa madereva wa bajaji na bodaboda kwa lengo la kuhimiza ushirikiano na umoja kati yao wenyewe na jamii inayowazunguka hasa kwenye swala la usalama barabarani
 7. Kuandaa, vitabu, makala na vipeperushi vya usalama barabarani
 8. Kutumia mitandao ya kijamii na vyombo vya habari
 9. Kutumia tovuti ya PESACO kutoa machapisho ya usalama barabari ikiwemo na tafiti za usalama barabarani.