Vizuizi kwa Dereva Barabarani
Vizuizi kwa Dereva Barabarani

Chochote ambacho kinaweza kuchukua umakini wako kwenye kuendesha chombo cha moto mfano gari  ukiwa barabarani  kinaweza kuwa kizuizi. Kutuma ujumbe mfupi wa maandishi, kuongea kwenye simu, kutumia mfumo wa urambazaji (GPS) na kula wakati unaendesha chombo cha moto, vyote hivi vinaweza kuchukua umakini wa dereva kwenye lengo lililompeleka barabarani na kuhatarisha maisha yake, abiria na watumiaji wengine wa barabara.    

Vizuizi vimegawanyika kataika sehemu tatu amabazo ni:- Kuona. Huchukua macho yako kutoka barabarani (mf. Vitu vya kutazama) Mikono Huchukua mikono yako kutoka kwenye usukani (mf. Kupokea, kuongea na kutumia simu barabarani, kula n.k) Utambuzi Huchukua akili yako barabarani (mf. Msongo wa mawazo)   

  

Vifuatavyo ni baadhi ya vizuizi kwa dereva awapo barabarani 

Matumizi ya simu wakati wa kuendesha chombo cha moto 

 Kutumia simu wakati unaendesha gari aidha kwa mkono au namna nyingine huongeza nafasi kubwa ya kusabaisha ajali. Kusoma au kutuma ujumbe wa maandishi  humfanya dereva atoe macho yake na akili barabarani  kwa zaidi au sekunde kadhaa akiwa anaendesha gari na kitendo hiki ni hatarishi kwa dereva na watumiaji wengine wa barabara. Unapotumia simu wakati unaendesha gari fikra au fahamu zako zote hutoka barabarani na kuhamia kwenye simu. Hali hii humpunguzia dereva ufanisi wa kumudu chombo chake akiwa barabarani na mwishowe anaweza kukosa mwelekeo na kusababaisha ajali. Wataalamu wanakadiria kwamba kuendesha gari kilometa 80 au zaidi kwa saa wakati unaaandika na kutuma meseji ni sawa na kuendesha gari kwa  umbali wa uwanja wa mpira (mita 100) wakati umefunga macho. Jambo muhimu ni kuchukua tahadhari kabla ya hatari, na tahadhari yenyewe ni kutokutumia simu kwa vyovyote vile wakati unaendesha gari hata kama umesimama kwenye taa nyekundu. Kama simu ni ya muhimu sana paki gari pembeni katika sehemu ambayo ni salama kisha ukimaliza enelea na safari yako.   

  Matumizi ya GPS 

 Kuweka au kutumia GPS kwenye simu yako ni hatari kama kutuma na kusoma meseji wakati uanaendesha gari. Hata kuangalia tu mwelekeo kwenye GPS kunaweza kusababisha majanga. Kama unaenda kutumia GPS hakikisha simu au kifaa unachotumia kimewekwa mahali ambapo unaweza kukiona kirahisi na kuongeza sauti ili uweze kusikiliza mwelekeo(direction) au kama kuna mtu pembeni yako akusadie kuangalia GPS au urambazaji.   


 Kuongea na abiria 

 Ni ngumu kutoongea kwa wale wanaoendesha gari na unaweza kuonekana wa ajabu usipofanya hivyo, ila kuongea, kucheka na kumuangalia abiria bado ni kizuzi cha kuendesha gari kwa umakini. Wataalamu wanasema dereva mwenye msafiri mmoja pembeni yake ana uwezekano wa mara mbili au zaidi kusababisha ajali kwa sababu kuongea kutakuwa kwingi na mbali na hilo mara nying mazungumzo yanaweza kuhusisha matumizi ya ishara. Jaribu kuweka mazungumzo yako kuwa mafupi na ambayo hayatachukua umakini wako barabarani.   


Kushughulika na watoto ndani ya gari au wanyama (mf. mbwa) 

 Siyo salama kumuacha mtoto au mnyama kuzunguka na kucheza kwenye gari. Jambo la hatari zaidi ni kwamba walio wengi hufanya hivyo na kutoa mwanya wa kusumbuliwa. Kila mzazi anajua namna gani watoto ni changamoto kwenye gari. Mtoto au mnyama anaweza kujaribu kuweka kichwa dirishani kwa lengo la kuchungulia. Huu ni usumbufu kwako kwa sababu utawajibika kumrudisha kwenye kiti  na wakati huo unaendesha gari. Njia salama ya kuepukana na usumbufu huu ni kuhakikisha mtoto anakaa kwenye kiti kwa utulivu na kumfunga mkanda wa usalama. Watoto wanahitaji umakini wa hali ya juu. Wakati mwingine wanaweza kupigana au kuhitaji chakula bila kujua wala kujali upo wapi na kwa hali gani. Haya yakiwa yanaendelea inaweza kua ngumu kwako dereva kutuliza akili yako barabarani. Kama unataka kusafiri na watoto au wanyama hakikisha wamekaa kwenye kiti kwa usalama. Jaribu kuwapa vyakula, maji, midoli au vitabu kabla hujaingia barabarani.   


  Kubadilisha mziki, redio au AC 

 Kunaweza kukawa na joto nje na ukahitaji kuwasha AC au mziki mzuri umechezwa na unataka kuongeza sauti. Inaweza kuonekana ni kitu kidogo sana ila kubadilisha kitu chochote kwenye gari wakati ukiwa unaendesha kunaweza kuchukua macho na umakini wako kwa sekunde kadhaa na muda huo unatosha kupelekea ajali. Unashauriwa kubiri mpaka gari lako lisimame au kama una gari jipya na la kisasa tumia vibadilishi vya kwenye usukani. Kusikiliza mziki au mpira kwenye gari ni sehemu mojawapo ya kizuizi kwa dereva. Mfano kuna madereva huendesha vyombo vya moto huku wameweka mziki kwa sauti kubwa, jambo hilo hupunguza umakini wao barabarani. Pia wale wanaosikiliza mpira huku wanaendesha vyombo vya moto tabia hiyo ni hatarishi sana hivyo unaaswa kulikataa, kulikemea na kutolifanya jambo hilo ukiwa unaendesha chombo cha moto.   


  Kula na kunywa 

 Wakati mwingine tunahitaji kula chakula cha haraka kwenye gari. Pamoja na hilo, hiyo sio sababu iliyokuweka barabarani. Kutafuna kitu chochote ni kizuizi ambacho inabidi kikwepwe iwezekanavyo. Na ikumbukwe kwamba matuta na ubovu wa barabara vinaweza kusababisha ukapaliwa na chakula hali ambayo inahatarisha usalama wako barabarani na wa watumiaji wengine wa barabara.   


Ndoto za mchana (kuwaza) 

 Hii ni kawaida kwa kila binadamu na inaweza kusababaisha ajali kwa sababu akili inatoka barabarani unapo kufikiria mambo mengine. Jitahidi kadri iwezekanavyo akili yako iwe barabarani na sio kwingine.   


Kupaka makeup 

 Baadhi ya watu hufikiria sana kuhusu mwonekano wao kabla hawajafika wanapoelekea, hilo linafahamika. Unataka kuonekana vizuri. Ila gari likiwa barabarani sio sehemu ya kuweka mascara, lipstick, blush au hata kuchana nywele zako. Angalau fanya hivyo wakati ukiwa hauendeshi gari(haupo barabarani). Na kama hujajipendezesha kabla ya kuondoka jitaidi mpaka ufike salama unapoenda na malizia shughuli yako baada ya kuegesha gari mahali salama.   


Kuvuta sigara 

 Kuwasha, kuweka majivu kwenye kisehemu chake na kushikilia sigara ni shughuli ambazo zinaweza kuchukua macho na umakini wako uwapo barabarani.   


Hisia 

 Kuendesha wakati ukiwa na huzuni, hasira na kuchanganyikiwa huweza kuwa kizuizi cha kuendesha kwa umakini ukiwa barabarani. Mf. Kama ikitokea mahusiano yako yakavunjika au hayapo kwenye muelekeo mzuri au umekuwa na siku mbaya kazini tulia kwanza kabla hujaingia barabarani. Mtafte hata rafiki wa karibu au ndugu yako fanya liwezekanalo kuweka hisia zako sawa ( zisiwe kikwazo ukiwa barabarani) au kama unadereva wako umuache akuendeshe.

PESACO TANZANIA