Watoto wadogo huhitaji msaada kutoka kwa watu wakubwa
pindi wakiwa kwenye mazingira ya barabara. Pia ni fursa kwao kujifunza kwa
vitendo kuhusu mazingira na mienendo ya barabarani wakiwa na wakubwa wao,
wazazi au walezi.Watoto wadogo hujifunza mienendo ya barabarani kwa kuangalia
na kufanya au kuigiza kama watu wengine wafanyavyo. Kwahiyo kuwa mfano mwema
kwao.Ongea na mwanao kuhusu barabara, alama, vyombo vya barabarani (mfano
magari na pikipiki), namna na wapi pa kuvuka barabara kwa usalama. Kwenye miaka ya mwanzo, watoto huhitaji msaada mkubwa kutoka
kwa wakubwa zao ili kuweza kukabiliana na hali ya barabarani kiujumla.
Wanahitaji msaada kutambua uwepo wa vyombo vya barabarani na madhara yanayo weza
kusababishwa na vyombo hivyo. Vile vile kuweza kutambua au kutabiri mwendo kasi na
umbali wa magari yanayokuja. Wakiwa wanakua na kuendelea kupata mafunzo au
maelekezo na ujuzi kutoka kwa jamii inayowazunguka, huwa na uelewa na wanaweza
kusimama kwa ajili ya usalama wao wenyewe wakiwa barabarani na kuwa watumia
barabara wanaofuata taratibu na kanuni za barabara. Ni vizuri mtoto kupata ujuzi kuhusu usalama barabarani akiwa
kwenye mazingira ya barabarani. Watoto hujifunza mambo mengi kwa kuona na kupitia
uzoefu. Muingiliano wa watoto na wakubwa huwasaidia kujifunza mengi kuhusu
barabara na usalama barabarani. Unaweza kuongea
na mtoto wako mkiwa manatembea, muulize
maswali kuhusu barabara, alama, magari, pikipiki n.k. Na namna gani na
wapi anaweza ukavuka barabara kwa usalama. Lengo la makala hii ni
kukufunza namna ya kumsaidia mtoto kuwa salama akiwa barabarani ikiwemo usalama
barabarani kwa watoto chini ya miaka mitano, watoto kati ya miaka mitano na
tisa na watoto kati ya miaka 10 mpaka 15. Uslama
barabarani kwa watoto chini ya miaka mitano Muda wote waelekeze watoto kwa umakini kuhusu hali ya
barabarani na ni muhimu kufanya yafuatayo:- Ø Ongea na mwanao kuhusu mazingira ya barabarani; Ø Mwanao akianza kutembea na wewe mwambie kwamba wakati
wote ashikwe mkono na wakubwa anaowafahamu pindi akiwa barabarani na kutembea
pembeni mwa barabara upande wa kulia au kwenye njia ya waenda kwa miguu. Ongea na
mwanao ni kwanini na kuna umuhimu gani kushikwa mkono akiwa barabarani; Ø Mwelezee kitendo au matendo yanayofanyika wakati mnavuka
barabara pamoja. Mhusishe mwanao kwenye kufanya maamzi kuhusu wakati salama wa
kuvuka barabara, pamoja na hili bado atakaye fanya maamzi ya kuvuka barabara ni
wewe ila kwa kitendo hicho utakuwa unampa mtoto uwezo wa kufikiri kwenye
mazingira ya barabarani; Ø Muda wote kuwa mfano mzuri kwa mwanao kwa kuvaa mkanda wa
usalama, kutii sheria na kanuni za barabarani, kuendesha kwa ufanisi na
utaratibu uliowekwa ukiwa barabarani; Ø Angaliana na watumiaji wengine wa barabara sana sana
kwenye makutano ya barabara; Ø Mhusishe mwanao kwenye kuchagua maeneo salama ya kucheza; Ø Vile vile mwelezee mwanao tofauti kati ya njia ya waenda kwa miguu na barabara, namna ya kutembea na mkubwa wanayemfahamu na
kushikana mikono pindi wakiwa karibu na barabara au barabarani, mueleweshe
maana ya simama, angalia, sikiliza na fikiri kwa vitendo, mwelezee ni maeneo
gani salama ya kuvuka barabara na kuwa mwangavu ili kuonekana na watumiaji
wengine wa barabara. Usalama
barabarani kwa watoto kati ya miaka mitano hadi tisa Mtoto wako bado anahitaji uangalizi na msaada akiwa
kwenye mazingira ya barabarani, hivyo fanya yafuatayo:- Ø Ongea na mwanao kuhusu alama za barabarani na taa za
barabarani, onesha na mwelezee maeneo salama ya kuvuka barabara; Ø Mfundishe mwanao namna ya kuvuka barabara kwa kutumia
‘simama, angalia, sikiliza na fikiri au tafakari’ ambapo atasimama kando ya
barabara, ataangalia na kusikiliza mtiririko wa magari na ataamua kama ni
salama kuvuka ama la. Panga safari nenda naye shuleni, pita njia salama ya kwenda
kwa miguu, na tumia sehemu salama kuvuka barabara kama vile vivuko vya waenda
kwa miguu na sehemu za barabara zilizo nyooka; Ø Mwelekeze mwanao njia nzuri na salama za kwenda na kurudi
kutoka shuleni; Ø Muda wote kuwa mfano mzuri, kwa mwanao kwa kuvaa mkanda
wa usalama, kufuata sheria na taratibu za barabarani na undeshaji wa kujihami. Ø Uliza shuleni kwa mwanao kuhusu miradi au mafunzo yanayoendeshwa
shuleni hapo kuhusu usalama baabarani kwa ajili ya wanafunzi. Usalama
barabarani kwa watoto kati ya miaka kumi
hadi kumi na tano Watoto kati ya miaka 10 na 15 wanaweza kumudu mazingira
ya barabarani. Ila hii itategemea na kiasi cha uelewa au uzoefu wa mtoto huyo
alicho nacho kuhusu mazingira ya barabarani. Nafasi ya mwanao kuumia akiwa barabarani kwenye umri
huu ni kubwa kuliko watoto wadogo, misukumo ya vijana wenzake inaweza kupelekea
tabia hatarishi wakiwa barabarani. Kundi hili linakuwa na uwezekano mkubwa wa
kupata ajali likiwa barabarani sababu ya safari ndefu kutoka mashuleni wakiwa
wenyewe na marafiki zao. Hivyo ni muhimu
kuzingatia yafuatayo:- Ø Hakikisha mwanao anaelewa umuhimu wa kutembea moja kwa
moja kuelekea nyumbani na sio vinginevyo; Ø Hata kama mwanao amefikia umri wa balehe endelea kuongea
nae kuhusu usalama barabarani, na hakikisha anafahamu na kuendelea kuchukua
tahadhari pindi akiwa barabarani; Ø Fuatilia na angalia kama mwanao muda wote husimama,
huangalia, husikiliza na kutafakari au kufikiri wakati akivuka barabara. Muulize
akuelezee nini anafanya na kwa nini anafanya hivyo akiwa barabarani; Ø Ongea na mwanao kuhusu sheria za barabarani. Nenda nae
ukiwa unaendesha gari kama itawezekana na tembea nae barabarani; Ø Panga na mwanao kuhusu njia salama kuelekea shuleni na
maeneo ambayo mwanao hutembelea mara kwa mara;