Mambo Yakuzingatia kwa Mtembea kwa Miguu Awapo Barabarani
Mambo Yakuzingatia kwa Mtembea kwa Miguu Awapo Barabarani

Kila mtu ana upendeleo wake likija swala la usafiri, ila ukweli ni kwamba kila mmoja hutumia miguu kama usafiri kutoka sehemu moja kwenda nyingine, “every one is naturally a pedestrian”. Barabara sio kwa ajili ya magari na pikipiki pekee bali hata waenda  kwa miguu. Takwimu zinaonyesha kua waenda kwa miguu ni miongoni mwa wahanga wakubwa wa ajali za barabarani. Hivyo ni muhimu kwa kila mtu kuwa na elimu stahiki ya namna yakutumia barabara wakati wakutembea.

 

Yafuatayo  ni mambo ya kuzingatia unapotembea barabarani;

1.    Tabirika, fuata sheria na taratibu za barabarani na tilia maanani alama, ishara na michoro ya barabarani;

2.    Pita kwenye njia za pembeni kama zipo;

3.    Tembea upande wa kulia mwa barabara ili uweze kuyaona vizuri na kupishana na magari yanayotoka unakoelekea na iwe pembeni sana iwezekanavyo

4.    Onekana muda wote, vaa nguo zinazong’aa wakati wa mchana na zinazo akisi mwanga wakati wa usiku au tumia tochi;

5.    Angalia magari yanayo ingia na kutoka barabarani au yanayo taka kuegesha au kutoka kwenye maegesho.

6.    Epuka ulevi wa aina yoyote ukiwa unatembea barabarani, itakupunguzia uwezo wa kufanya maamuzi;

7.    Kuwa makini muda wote, vyombo vya kielektroniki visikuchanganye, kawaida vyombo hivyo huchukua masikio na macho yako barabarani, mfano “earphones” au “headphones”.

 

 

Madhara ya kuweka “earphones” au “headphones” masikioni uwapo barabarani

·       Hutosikia mingurumo ya gari hali inayoweza kukusababishia kupata ajali;

·       Huhamisha akili yako kwenye kile unachokisikiliza zaidi hivyo unaweza kujisahau kufuata kanuni na tarabibu stahiki uwapo barabarani;

·       Ukipata taarifa ya mshtuko huenda ikakuathiri. Hasa kama ulikua unatumia simu.

 

Kuvuka barabara

a)    Tafuta sehemu salama ya kuvuka

b)   Fuata kanuni  za kuvuka barabara-

 

Sehemu salama kuvuka barabara

·       Mahali ambapo kuna afisa wa polisi au mtu yeyote mwenye mamlaka anaeongoza magari. Kumbuka kuwa ishara na maelekezo ya askari yanapaswa kupewa kipaumbele. Na mara zote vuka mbele yao;

·       Kwenye eneo ambalo kuna kivuko cha waenda kwa miguu (alama ya punda milia);

·       Kwenye taa za barabarani ambazo utafuata ishara za taa hizo;

·       Madaraja ya waenda kwa miguu na njia za chini;

·       Sehemu ambapo unaweza kuona pande zote na ambapo watumiaji wengine wa barabara wanaweza kukuona vizuri.

 

Sehemu ambazo siyo salama kuvuka barabara

·       Sehemu ambapo kuna kizuizi kinachokuzuia kuona barabara vizuri pande zote. Mfano eneo ambalo gari au magari yameegeshwa kama vile kwenye kituo cha mabasi;

·       Usivuke barabara kwenye makutano ya barabara au njia panda;

·       Usivuke barabara kwenye kona;

·       Usivuke mbele ya magari ya dharura. Iwapo utayaona au kuyasikia magari ya wagonjwa, magari ya zima moto, ya polisi au magari mengine yeyote ya dharura yenye vimulimuli  na sauti za ving’ora, usivuke barabara mpaka yapite;

·       Kamwe usivuke barabara moja kwa moja nyuma au mbele ya basi. Usivuke barabara na basi. Acha mpaka lipite ili uweze kuona pande zote za barabara vizuri;

·       Usipande juu ya uzio. Katika sehemu zingine za barabara uzio umewekwa ili kuwazuia watembea kwa miguu kuvuka barabara na kuwaongoza mahali salama pa kuvuka. Usipande juu ya uzio, au kutembea katikati yake na barabara. Vuka kwenye nafasi iliyowekwa.

 

Fuata kanuni za kuvuka barabara

·       Simama kwenye ukingo wa barabara;

·       Angalia magari barabarani, upande wa kulia, kushoto, kulia tena sehemu zote kuzunguka, na sikiliza mgurumo wa gari;

·       Kama kuna gari linakuja liache lipite;

·       Angalia tena upande wa kulia, kushoto kulia tena;

·       Baada ya kufanya maamuzi ya kuvuka usitabiri kwamba dereva anakuona, wakati mwingine inawezekana asikuone, kwa hiyo umakini ni juu yako na wakati wa kuvuka hakikisha macho yako na ya dereva yamekutana na ameonesha dalili za kukuruhusu uvuke mfano, kupunguza mwendo au kusimama;

·       Kuvuka kwenye taa za barabarani. Katika baadhi ya sehemu kuna ishara za taa za barabarani zinazo ongoza magari wakati wa kusimama na watembea kwa miguu wakati wa kuvuka. wakati ishara ya mtu aliyewima mwenye rangi nyekundu inapooneshwa USIVUKE. Wakati taa zikibadilika kuonesha ishara ya mtu anayetembea mwenye rangi ya kijani, angalia kuwa magari yamesimama na kisha vuka kwa uangalifu. Baada ya muda ishara ya rangi nyekundu, au wakati mwingine ishara ya rangi ya kijani inawaka gafla, na hii maana yake usianze kuvuka, kwasababu magari karibu yataanza kwenda tena. Iwapo taa za barabarani hazina ishara maalumu kwa watembea kwa miguu, angalia kwa umakini na usivuke hadi taa nyekundu itakapowaka na magari kusimama. Pamoja na hayo angalia magari yanayopinda kona. Kumbuka kuwa taa za barabarani zinaweza kuruhusu magari kutembea kwenye baadhi ya njia wakati njia zingine zikiwa zimesimama.

·       Kabla hujavuka hakikisha unatazama kulia , kushoto , kulia tena, ikiwa ni salama na umejiridhisha kuwa utavuka salama basi vuka barabara kwa umakini na uvuke kwa kunyooka usivuke barabara kwa mshazari wala kwa kukimbia, endelea kutazama magari wakati unavuka barabara. 

Shirika La Elimu ya Utekelezaji wa Sheria