Taa za barabarani ni moja ya ishara za usalama barabarani
na zipo kwa mujibu wa sheria ya usalama bararani sura ya 168 ya mwaka 2002. Taa za barabarani maranyingi hufungwa pembeni,
au katikati ya barabara kwa lengo la kuongoza mserereko wa magari barabarani
pamoja na kuweka uwiano sawa wa matumizi ya njia kwa makundi yote ya watumia
barabara, kama wenye vyombo vya moto, waenda kwa miguu, waendesha baiskeli,
wasukuma mikokoteni. Kwa mujibu wa sheria ya usalama barabarani ya mwaka 2002
sura ya 168 kifungu No. 73(2) watumiaji wote wa barabara wanatakiwa kuheshimu
na kufuata ishara zinazooneshwa na taa za barabrani.
Aina za Taa za Barabarani
Nyekundu
Taa nyekundu barabarani huonesha ishara ya SIMAMA. Vyombo
vya moto nyote barabarani vinalazimika kusimama pale rangi ya taa zinazoongoza
vyombo hivyo pamoja na watumiaji wengine wa barabara kuonesha rangi nyekundu.
Kwa mujibu wa sheria ya usalama barabarani ni kosa kisheria kuvuka taa
nyekundu. Mbali na kuwa ni kosa pia ni hatari kutumia barabara kwa wakati huo
kwasababu unaweza kusababisha ajali. Hii ni kutokana na kuwa ishara
inayoonekana na taarifa inayotolewa kwa wakati huo ni kuwa siyo zamu yako
kutumia barabara kwa wakati huo bali ni zamu ya watumiaji wengine. Wanaweza
kuwa waenda kwa miguu au ni wakati wa U-turn au makutano ya barabara. Katika
mazingira hayo ni rahisi ajali kutokea.
Kwa vivuko vya waenda kwa miguu vinavyoongozwa na taa,
waenda kwa miguu pia wanalazimika kusimama
pale mtu wa rangi nyekundu anapooneshwa kwenye taa. Lakini pale ambapo mwenda
kwa miguu anataka kukatiza bararaba na sehemu hiyo haina alama ya punda milia,
anatakiwa kukatiza barabara pale ambapo taa inaonesha rangi nyekundu na magari
yote yamesimama kutoka pande zote. Wakati wa kuvuka ni lazima atumie kanuni za
uvukaji salama wa barabara.
Mshale mwekundu pia unakuwa na maana ile ile kuwa
unatakiwa kusimama hadi pale mshale wa kijani utakapoonekana.
Njano
Taa ya njano hutoa ishara ya “TAHADHARI” na “JITAYARISHE
KUSIMAMA”. Maana ya taa hii ni kuwa jitayarishe kusimama kwasababu taa nyekundu
ipo karibu kuwaka. Ni wajibu wa dereva kusimama anapoona taa ya njano iwapo ni
salama kufanya hiyo, yaani unauwezo wa kusimama bila kusababaisha usumbufu au
hatari yoyote barabarani kwa wakati huo. Lakini endapo umekwisha ikaribia taa
na kwa wakati huo ameona kuwa siyo salama kusimama basi sheria inakuruhusu
kupita.
Mshale wa njano unamaana ya kuwa punguza mwendo na simama
mshale mwekundu upo karibu kuwaka.
Kijani
Taa hii inamaana ya NENDA. Lakini kabla ya kuondoka ni
wajibu wako kuhakikisha wanaovuka na kutumia barabara kwa wakati huo wamepita.
Mfano kwenye makutano ya barabara au kwenye U-turn magari yote yamepita
barabarani. Kwenye vivuko vya waenda kwa miguu vinavyoongozwa na taa,
wanapotaka kukatiza barabara ni sharti wasubiri mpaka mtu wa rangi ya kijani
anapoonekana kwenye taa.
Mshale wa kijani una maana ileile ya kupita uelekeo ule
tu ambao unaoneshwa kwenye mshale, inaweza kuwa kushoto ama kulia. Angalizo ni
kuwa kabla hujapinda kulia au kushoto sawasawa na mshale unavyokuongoza ni
lazima uhakikishe kuwa magari na watumiaji wengine wa barabara wamesimama na
hawapo barabarani kwa wakati huo.
Kwa mujibu wa sheria ya usalama barabarani ya mwamka 2002
sura ya 168 kifungu cha 73(4) sehemu
ambazo kuna taa, michoro na ishara za usalma barabarani lakini pia kuna askari
wa usalama barabarani, sheria inasema kuwa kwa wakati huo ishara na maelekezo
ya askari wa usalama barabarani ndiyo yanatakiwa kufuatwa nakupewa kipaumbele.
NB
Endapo taa za barabarani zimezima kwa wakati huo kutokana
na tatizo la kiufundi au umeme kukata watumiaji wote wa barabara wanaaswa
kutumia njia kwa zamu. Ni lazima kusimama unapokaribia makutano ya barabara ili
kutoa nafasi kwa wanaotumia njia kwa wakati huo na zamu yao inapoisha basi ni
zamu yako kutumia njia kwa wakati huo. Ni lazima pia kutumia njia kwa uangalifu
mkubwa maeneo ya makutano ya barabara na endapo taa za barabarani zimezima na
hakuna askari au mtu mwenye mamlaka kisheria kuongoza magari.